Takriban wanawake 50 hufariki kila mwaka kutokana na changamoto za uja uzito katika kaunti ya Migori, hayo ni kulingana na mtaalam wa uzazi Dkt Daniel Agullo.
Licha ya ushirikiano kati ya wizara ya afya na sekta ya kibinafsi, maafa kutokana na changamoto za uja uzito yanazidi kuongezeka, na kuibua wasi wasi miongoni mwa maafisa wa afya katika eneo hilo.
Kulingana na Dkt. Agullo, maafa hayo yanasababishwa na ukosefu wa huduma bora za matibabu na miundomsingi inayohitajika ya afya.
Aidha kulingana na ripoti ya Dkt. Agullo, usambazaji usio sawa wa maafisa wa afya pia umesababisha ongezeko hilo, akidokeza kuwa wahudumu wengi wa afya hupelekwa mijini na kuwaacha wakazi wa mashinani wakitaabika.
Alitoa wito kwa asasi husika kuhirikiana kwa karibu na wataalam wa afya, ili kuhakikisha wakazi wa maeneo ya mashinani wanapata huduma bora za afya, ili kukabiliana na maafa hayo.