ICTA, Microsoft zasaini mkataba wa kuharakisha mabadiliko ya kidijitali

Martin Mwanje
2 Min Read
Mamlaka ya Habari, Teknolojia na Mawasiliano, ICTA leo Jumanne imetia saini mkataba wa makubaliano na kampuni ya Microsoft katika hafla iliyoshuhudiwa na Katibu katika Idara ya ICT na Uchumi wa Dijitali Mhandisi John Tanui.
Mkataba huo unalenga kuongeza kasi ya mabadiliko ya kidijitali nchini na unanuia kuisaidia serikali ya Kenya kufikia malengo ya Mwongozo wa Uchumi wa Kidijitali.
Microsoft itashirikiana na serikali kuu, wizara, idara na taasisi kupitia ICTA katika mpangokazi wa pamoja unaotarajiwa kumaliza kufanyiwa kazi mnamo mwezi Februari mwakani.
Chini ya makubaliano hayo, Microsoft itaisaidia serikali na jukumu la kukumbatia mkakati wa kutoa kipaumbele kwa matumizi ya mtandao kupitia matumizi ya teknolojia na kuboresha utendakazi kupitia utoaji huduma za serikali kwa raia kupitia mtandaoni.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu Tanui aliisifia ICTA na Microsoft kwa ushirikiano huo, akiutaja kuwa mtazamo muhimu katika kuharakisha uchumi wa dijitali wa nchi ambao tayari umepiga hatua kubwa.
“Kama nchi, tumeweka msingi wa mazingira bora ya uchumi wa dijitali unaohitaji washikadau kama nyinyi kusaidia katika kuendeleza sekta yetu,” alisema Mhandisi Tanui.
“Hadi kufikia sasa, tumeweka huduma za serikali zaidi ya 14, 000 mtandaoni na ushirikiano huu ni muhimu katika kuendeleza uchumi wetu wa dijitali.”
Kunle Awosika, Mkuu wa Sekta ya Umma barani Afrika katika kampuni ya Microsoft alisema kampuni hiyo imefurahia kuingia katika ushirikiano huo unaotafuta kubuni mazingira ya wazi na wezeshi kwa idara za serikali.
Website |  + posts
Share This Article