Ichung’wa: Madai ya Raila kuhusu mpango wa uagizaji mafuta ni propaganda

Tom Mathinji
3 Min Read

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wa amepuuzilia mbali madai ya kiongozi wa upinzani Raila Ondiga, aliyeshutumu mfumo wa uagizaji bidhaa za mafuta kati ya serikali ya Kenya na Saudi Arabia.

Kupitia taarifa aliyopachika katika mtandao wake wa X awali ukijulikana twitter, Ichung’wa alitaja madai ya Raila kuwa propaganda za kisiasa na ni njama za kufufua umaarufu wake wa kisiasa ambao umedidimia.

“Madai ya Raila Odinga  ni propaganda za kisiasa na uvumi. Madai hayo hayana msingi wala ushahidi,” alisema  Ichung’wa.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga hapo awali, alidai kuwa Kenya haijatia Saini mkataba wowote na muungano wa Milki za kiarabu au Saudi Arabia, mbali mkataba huo ulikuwa ni baina ya wizara ya nishati ya Kenya na kampuni za mafuta zinazomilikiwa na serikali za Mashariki ya kati

Madai ya Odinga kwamba mfumo wa serikali kwa serikali wa kuagiza mafuta unaotekelezwa na utawala wa Rais William Ruto, unaongeza bei ya mafuta na kuwafaidi baadhi ya maafisa wa serikali, yalipingwa vikali na Ichung’wa, yakitajwa yasiyo na msingi wowote.

Kulingana na mbunge huyo wa eneo bunge la Kikuyu, kampuni zilizotajwa na Odinga za Gulf Energy, Galana Oil Kenya Ltd na Oryx Energies Kenya Ltd,  sio mawakala wa serikali ya Ake ya mbali zinawakilisha kampuni za mafuta za mataifa ya kiarabu.

“Bwana Odinga anadokeza kuwa wizara ya Kenya ya nishati na petroli, ilitia Saini mkataba na kapuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali Mashariki ya kati. Ikiwa huo sio mkataba baina ya serikali mbili, basi mkataba uliotiwa saini kati ya wizara ya serikali na shirika la serikali ni nini?,” aliuliza Ichung’wa.

Aidha Ichung’wa alimshutumu Odinga kutokana na masaibu yanayokumba sekta ya mafuta, kufuatia kuwekwa ruzuku kwa bidhaa za mafuta, baada ya maridhiano kati yake na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Si haki Kwa mwanasiasa aliye na hadhi kama ya Raila Odinga kutafuta umaarufu wa kisiasa kutokana na matatizo yeye na mshirika wake wa maridhiano waliyosababisha,” alidokeza Ichung’wa.

Ichung’wa alimuonya Raila dhidi ya kumhusisha Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika sakata hiyo ya mafuta, baada ya Odinga kudai kuwa taifa moja jirani linatafuta njia mbadala za kuagiza mafuta kwa kuwa mawakala wa Kenya wanaongeza bei ya bidhaa za mafuta.

“Mpango wa kuagiza mafuta baina ya serikali, hauna madhara yoyote kwa Uganda, kwa kuwa Uganda hununua bidhaa za mafuta kwa njia huru na husafirishia bidha hizo kupitia Kenya,” alisema mbunge huyo wa Kikuyu.

Website |  + posts
Share This Article