Ibada ya waliofariki kwenye ajali Nyeri kuandaliwa Jumanne ijayo

Kati ya watu 16 waliofariki, 11 ni wa kutoka kaunti ya Nyeri huku waliosalia wakitokea kaunti za Meru, Kitui, Kirinyaga, Kiambu na Machakos.

radiotaifa
1 Min Read

Ibada ya kuwakumbuka watu 16 waliofariki katika ajali kwenye barabara kuu ya Nyeri-Nyahururu Jumamosi wiki iliyopita itaandaliwa Aprili 7 mwaka huu.

Ibada hiyo itaandaliwa katika uwanja wa Nyeri ASK Kabiru-ini na itahudhuriwa na wakazi na viongozi mbalimbali wa eneo hilo wataofika kuwapa mkono wa buriani marehemu.

Akitangaza hayo, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga amesema miili yote 16 imetambuliwa na jamaa.

Kati ya watu 16 waliofariki, 11 ni wa kutoka kaunti ya Nyeri huku waliosalia wakitokea kaunti za Meru, Kitui, Kirinyaga, Kiambu na Machakos.

Gavana Kahiga amesema kaunti yake tayari imeweka mipango ya familia zilizofiwa kupokea ushauri nasaha ili kuzisaidia kukabiliana na msiba huo.

Ameongeza kwamba kamati ya pamoja ya maandalizi itagharimia mazishi hayo ikiwa ni pamoja na ada ya upasuaji wa miili.

Upasuaji huo ulioanza jana Jumanne katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Nyeri utakamilika kesho Alhamisi.

Wakati huohuo, manusura 6 wa ajali hiyo wako katika hali thabiti na wanaendelea kupata nafuu katika hospitali mbalimbali.

Taarifa ya KNA

Share This Article