Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Extreme Sports Limited Hussein Mohammed ameelezea matumaini ya Waziri wa Michezo Ababu Namwamba kurejesha hadhi ya soka nchini.
Akizungumza Alhamisi alipohutubia kongamano la Afrika kuhusu kandanda, Hussein pia alisisitiza haja ya kuzingatia zaidi uwekezaji katika soka ya mashinani ikiwa ndio njia pekee ya kukuza kandanda nchini na kupata vikosi thabiti katika timu zote za taifa.
“Soka ya mashinani ndio nguzo ya pekee itakayotusaidia kuinua viwango vya mpira nchini na pia barani Afrika. Mpira wetu umekabiliwa na changamoto si haba kutoka miundombinu duni, mikakati ya pata potea ya kukuza mchezo pamoja na usimamizi mbaya, hali ambayo pia inashuhudiwa katika mataifa mengine ya Afrika,” alisema Hussein.
“Waziri wa Michezo Ababu Namwamba kwa wakati fulani ameelezea FIFA, na pia kuhusu maovu ya usimamizi wa sasa wa kandanda. Wadau bado wanasubiri majibu ya FIFA.”
Kongamano la biashara ya soka barani Afrika mwaka 2023 limeandaliwa na wakfu wa soka barani Afrika, na limewaleta pamoja wadau wa soka kujadiliana fursa zilizopo katika kandanda.
Hussein ni mwasisi wa mashindano ya soka ya ligi ya Super 8 iliyoadhimisha miongo miwili maajuzi tangu kuzinduliwa.