Huduma za kawaida zarejelewa KNH baada ya hitilafu ya mfumo

Wagonjwa kadhaa walifika katika afisi za wizara ya Afya kudai majibu wakisema wametatizika mno kupata huduma kutokana na kutopatikana kwa mfumo wa SHA katika hospitali ya Kenyatta.

Marion Bosire
1 Min Read

Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta KNH imethibitisha kurejelewa kwa huduma za kawaida hospitalini humo baada ya kulemazwa kwa muda na hitilafu ya mfumo.

Hitilafu hiyo inasemekana kuathiri huduma katika taasisi hiyo ya kutegemewa nchini kwa muda wa siku mbili.

Mfumo wa Halmashauri ya afya ya jamii SHA ulikosa kuwiana na ule wa hospitali kuu ya Kenyatta lakini sasa kila kitu kimerekebishwa kulingana na afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo Evanson Kamuri.

Katika taarifa Daktari Kamuri aliomba radhi kutokana na kucheleweshwa kwa huduma za usimamizi wa wagonjwa, huku akitoa hakikisho kwamba huduma sasa zinapatikana kwa njia shwari.

Katika kushughulikia tatizo hilo, mkuu huyo wa KNH alielezea kwamba walilazimika kuongeza wahudumu katika idara zilizoathirika na kuongeza muda wa kazi.

Kamuri alitoa hakikisho kwamba wamejitolea kushughulikia masuala yote yaliyosalia kwa njia inayofaa.

KNH ambayo ndiyo hospitali kuu ya rufaa imetoa hakikisho la huduma bora huku ikishukuru wananchi kwa kuwa na subira na uelewa wakati tatizo hilo lilitokea.

Haya yanajiri saa chache baada ya wagonjwa kadhaa kuingia kwa kishindo katika afisi za wizara ya Afya kudai majibu wakisema wametatizika mno kupata huduma kutokana na kutopatikana kwa mfumo wa SHA katika hospitali ya Kenyatta.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *