Huduma ya Taifa ya Polisi yakanusha kuhusika katika utekaji nyara

Katika taarifa ya leo iliyotiwa saini na Inspekta Jenerali Douglas Kanja, NPS imeelezea kutoridhishwa na taarifa zinazosambazwa ikizitaja kuwa za uongo.

Marion Bosire
1 Min Read
Douglas Kanja - Inspekta Mkuu wa Polisi

Huduma ya Taifa ya Polisi nchini, NPS imekanusha madai kwamba maafisa wa polisi wanahusika katika visa vya utekaji nyara vinavyoshuhudiwa nchini.

Katika taarifa ya leo iliyotiwa saini na Inspekta Jenerali Douglas Kanja, NPS imeelezea kutoridhishwa na taarifa zinazosambazwa ikizitaja kuwa za uongo.

Kanja alifafanua kwamba mamlaka ya maafisa wa polisi yanahusu tu kukamata wanaovunja sheria kwa njia inayokubalika kisheria na wala sio kuwateka nyara.

“Mchakato kulingana na sheria za huduma uko wazi: shughuli zote za kukamata wahalifu lazima zinakiliwe kwenye kitabu cha matukio ili wafikishwe mahakamani baadaye.” alielezea Kanja kwenye taarifa yake.

Alisema iwapo mtu hatafikishwa mahakamani basi anafaa kuachiliwa huru.

Huduma ya taifa ya polisi imefafanua pia kwamba waliotekwa nyara hawazuiliwi kwenye kituo chochote cha polisi kote nchini.

Huku akitambua kwamba Kenya ni nchi ya kidemokrasia ambayo ina haki ya uhuru wa kujieleza, Kanja alishauri kwamba uhuru huo wa kijieleza una viwango fulani na unafaa kutumiwa kwa kuwajibika.

Amesihi umma ukome kusambaza taarifa ambazo hazijadhibitishwa zinazolenga kuchafua sifa za huduma ya taifa ya polisi.

Kulingana na Kanja suala hilo la utekaji nyara tayari linachunguzwa na mamlaka ya kutathmini utendakazi wa polisi IPOA na anaomba taarifa za waliotoweka kuwasilishwa kwenye vituo vya polisi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *