Huduma Kenya yasema agizo la Rais la vitambulisho kutolewa bila malipo linasalia

Marion Bosire
2 Min Read

Usimamizi wa vituo vya Huduma Kenya umefafanua kwamba agizo la Rais William Ruto kuhusu utoaji bila malipo wa vitambulisho vya kitaifa kwa wanaotaka nakala baada ya vitambulisho vyao kupotea au kuharibika linasalia.

Katika taarifa kwa umma, Huduma Kenya ilielezea kwamba agizo hilo la Rais  halijakanganywa kwa vyovyote. Taarifa hiyo ilielezea kwamba utekelezaji wa agizo hilo unaendelea huku taasisi hiyo ikishukuru wananchi kwa subira yao.

Rais Ruto jana Oktoba 28, 2025 alielekeza kwamba malipo ya shilingi elfu moja ambayo hutozwa waliochukua vitambulisho awali na wanataka nakala nyingine yaondolewe ili kuhakikisha kila mmoja anajisajili kama mpiga kura.

Kiongozi wa nchi alisema malipo hayo yataondolewa hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, kama njia ya kuhakikisha hakuna anayefungiwa nje ya shughuli hiyo muhimu.

Lakini inaonekana agizo lake halijaanza kutekelezwa rasmi kwani Huduma Kenya awali ilielezea kwamba bado wanaotaka nakala za vitambulisho wanahitajika kulipa shilingi elfu moja kila mmoja.

Taasisi hiyo ilisema kwamba ilikuwa ikisubiri mawasiliano rasmi ya hatua hiyo kupitia arifa ya gazet rasmi la serikali.

Katika taarifa ya hivi punde zaidi, Huduma Kenya inasema haijakanganya au kukiuka agizo la Rais bali ni kwamba mchakato wa utekelezaji unaendelea.

Imeelezea kwamba mabadiliko ya kiutawala na kimfumo yanafanywa ili kuwezesha utekelezaji huo.

Website |  + posts
Share This Article