Chama cha Hospitali za kibinafsi za vijijini na mijini humu nchini (RUPHA), kimetangaza kusitisha huduma za halmashauri ya Afya ya Jamii (SHA) kuanzia Jumatatu wiki ijayo.
Kulingana na chama hicho, hatua hiyo inatokana na matatizo ya mfumo huo, malimbikizi ya malipo ya hazina ya zamani ya NHIF na mfumo wa malipo kwa wagonjwa wanaotibiwa na kwenda nyumbani usiotekelezeka.
Akihutubia wanahabari hii leo Alhamisi, mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Brian Lishenga, alisema changamoto zinazouzingira mfumo wa utoaji huduma za matibabu zimepuuzwa na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.
Lishenga aliongeza kwamba matatizo ya kila mara ya mfumo huo na ukosefu wa suluhu kutoka kwa halmashauri hiyo, sasa yanatishia uwepo wa vituo vya afya kutokana na utoaji wa huduma duni.
“Haikuwa rahisi kuafikia uamuzi huu. Ulitokana baada ya miezi kadhaa ya kukosa kutimizwa kwa ahadi na ongezeko la malimbikizi na hivyo kuhatarisha taasisi za afya hapa nchini,” alisema Lishenga.
Dkt. Lishenga alisema kwamba asilimia 54 pekee ya hospitali hazijapokea malipo kutoka kwa SHA, asilimia 89 ya vituo vya afya vimeripoti matatizo ya mtandao wa SHA huku asilimia 83 ya hospitali zikiripoti matatizo sugu katika kutathmini uwazi wa mgonjwa kutokana na changamoto za mifumo ya SHA.
RUPHA sasa inaitaka serikali kulipa malimbikizi ya deni la shilingi bilioni 30 kwa NHIF, kurejelea na kurahishisha mfumo wa SHA kwa wagonjwa wanaotibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani pamoja na kuhakikisha malipo kwa kuzingatia muda chini ya shirika la wasimamizi wa masuala ya matibabu nchini.
“Tunadaiwa madeni ambayo ni ya tangu mwaka 2017, hospitali hazijalipa mikopo ya benki na hazina dawa muhimu huku madaktari wengi wakikosa kulipwa,” alisema Dkt. Lishenga.