Hoja ya kumbandua Gachagua: Vikao vya kukusanya maoni ya Wakenya vyaanza

Martin Mwanje
2 Min Read
Wakazi wa Kakamega wakitoa maoni kuhusu hoja ya kumbandua madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua

Vikao vya kusikiliza kauli za Wakenya juu ya hoja maalum ya kumtimua madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua vimeanza katika kaunti zote 47 nchini leo Ijumaa. 

Hoja hiyo iliwasilishwa katika Bunge la Taifa Jumanne wiki hii na mbunge wa Kibwezi Magharibi Eckomas Mwengi Mutuse.

Iliorodhesha mashtaka 11 ya ni kwa nini Gachagua hapaswi kamwe kushikilia wadhifa huo.

Katika kaunti ya Nairobi, ukumbi wa Bomas umefurika raia wanaotoa maoni mseto, baadhi wakiunga mkono na wengine kupinga vikali hoja hiyo.

Katika kaunti ya Uasin Gishu, wakazi pia walijitokeza kwa wingi katika ukumbi wa serikali ya kaunti hiyo kuelezea hisia zao kuhusiana na mchakato unaoendelea.

Hali sawia imeshuhudiwa katika kaunti ya Kakamega ambako ukumbi panakofanyika mkutano huo ulifurika asubuhi na mapema.

Mikutano ya kukusanya maoni ya Wakenya pia inaendelea kaunti za Kajiado, Meru, Mombasa na kaunti zinginezo nchini.

Wakenya wameruhusiwa kutoa maoni juu ya hoja hiyo kwa mujibu wa kifungu 118 cha katiba ya nchi.

Jaribio la Naibu Rais jana Alhamisi kutaka mahakama kuzuia zoezi hilo la ukusanyaji maoni ya Wakenya lilishindikana baada ya mahakama kuagiza kuwa kesi hiyo itajwe Oktoba 9 mwaka huu.

Kufikia wakati huo, kesi hiyo huenda ikawa imepitwa na wakati kwani wabunge Oktoba 8 watakuwa wamesikiliza misingi ya mbunge Mutuse kuiwasilisha hoja hiyo na hata kuipigia kura ama kumtimua au kumdumisha Naibu Rais madarakani.

Ikiwa utapitishwa katika Bunge la Taifa, mswada huo pia utapelekwa katika Bunge la Seneti ili kutafuta idhini ya bunge hilo.

Ikiwa pia utapitishwa katika bunge hilo, basi itakuwa rasmi kwamba Naibu Rais ametimuliwa madarakani.

Katika Bunge la Taifa, wabunge 291 walitia saini hoja ya kutaka Gachagua atimuliwe mahakamani.

Ili hoja hiyo ipite katika bunge hilo, wabunge 233 wanahitajika kuiunga mkono hoja hiyo.

 

Share This Article