Kelvin Kiptum Cheruiyot alizaliwa Disemba 2,mwaka 1999 katika kijiji cha Chepsamo eneo la Chepkorio, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.
Alikuwa mwanariadha wa mbio za marathon ambapo anashikiliia rekodi ya Dunia.
Rekodi hiyo ilimfanya awe mwanariadha wa kwanza kutimka mbio za Nyika chini ya saa mbili na dakika moja.
Kiptum alikuwa na kaka wawili na dada wawili.
Wazazi wake walipenda michezo ambapo babake alikuwa mwanariadha huku mamake akishiriki mchezo wa voliboli wakati wa ujana wao.
Mwanariadha huyu alishiriki riadha ya mbio za kulipwa kwa mara ya kwanza mbio za kilomita 21 za Benki ya Family mjini Eldoret mwaka 2023 na kumaliza nambari ya 10.
Alikuza talanta yake zaidi akiwa shule ya upili ya wavulana ya Iten akiwa chini ya mkufunzi Brother Colm O’Connell ambaye ni kocha anayesifika kwa kuwanoa wanariadha wa Kenya.
Machi mwaka wa 2019, alikimbia mbio za kimataifa kwa mara ya kwanza nchini Ureno katika mbio za Lisbon Half Marathon alipomaliza wa tano na kuweka muda bora wake wa dakika 59:54.
Mwaka wa 2020, alianza kufanya mazoezi yake chini ya kocha kutoka Rwanda Gervais Hakizimana ambaye ni bingwa wa mita 3000 kuruka viunzi na maji.
Disemba mwaka wa 2020, alishiriki mbio za kilomita 21 za Valencia alipomaliza wa sita na muda wa 58:42 na kuweka muda wake bora.
Mwaka wa 2021, alikimbia nusu marathoni za Lens, nchini Ufaransa na Valencia Uhispania na kuweka muda wa 59:35 na 59:02 akimaliza katika nafasi za nne na nane mtawalia.
Mwaka wa 2022 ulikuwa wa Kiptum kwa kuwa kwa mara ya kwanza alishinda mbio za Valencia akitumia muda wa saa 2:01:53, Muda huo ulikuwa wa nne duniani ambapo ulimfanya kuwa mwanariadha wa tatu kukimbia chini ya saa mbili na dakika mbili.
Nyota ya Kiptum iliendelea kung’aa katika mbio za masafa marefu akishinda London Marathon mwezi Aprili mwaka wa kwa muda was aa 2:01:25.
Baadaye Oktoba 8, 2023, Kiptum alivunja rekodi ya dunia katika katika mbio za Chicago alipoweka muda wa saa 2:00:35.
Hadi kifo chake, Kiptum alikuwa akijitayarisha kushiriki mbio za nyika za Rotterdam nchini Uholanzi mwezi Aprili mwaka huu, kabla ya kushiriki michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Kiptum alifariki dunia katika ajali ya barabarani akiwa na kocha wake Hakizimana usiku wa Februari 11, 2024 baada ya Gari lake kupoteza mwelekeo kwenye barabara ya Eldoret – Ravine katika eneo la Kaptagat na kuwauwa papo hapo.
Abiria wa kike aliyekuwa kwenye gari hilo alinusurika na majeraha mabaya na kukimbizwa hispitalini.
Marehemu amemwacha mjane Asenath Rotich na watoto wawili.