Serikali ya kaunti ya Kilifi imeungana na washikadau wengine katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Kulingana na takwimu kutoka Idara ya Jinsia, Utamaduni na Huduma kwa Jamii kaunti ya Kilifi, watoto, wanawake na wanaume pamoja na wazee hupitia changamoto hiyo huku watu watatu kati ya kumi wakiathirika.
Kulingana na Afisa Mkuu wa idara hiyo Agneta Karembo, visa vingi vimekuwa vya mauaji ya wazee sambamba na unyanyapaa kutokana na kupigwa kwa waume na wanawake.
Kama juhudi ya kukomesha changamoto hizo, serikali ya kaunti ya Kilifi ikishirikiana na washikadau wengine sasa imezindua kampeni almaarufu Red Card Campaign ambapo sanaa hutumika katika kuwaelimisha jamii umuhimu wa kuzingatia sheria na maadili mema na kutojihusisha na ukatili wa kijinsia.