Jumla ya mikwangurano mitatu ya raundi ya tano, hatua ya makundi kufuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwaka 2024, zitapigwa Jumatano.
Sudan Kusini itakuwa mwenyeji wa Gambia kundini G .
Sudan Kusini hawana budi kushinda mchuano huo ili kufufua matumaini ya kufuzu wakishika nanga kwa pointi tatu, wakati wapinzani wao Gambia wakiwa na alama 6 na ushindi ugenini utawaweka guu moja ndani ya kipute cha mwakani.
Katika kundi A, Sao Tome and Principe watamenyana na Guinea Bissau huku Guinea wakiwaalika Misri ugani Marakesh nchini Morocco katika pambano la kundi D.
Sare itazifuzisha timu zote kwa patashika ya mwaka ujao nchini Ivory Coast, zikiwa sako kwa bako pointi tisa kila moja baada ya mechi nne.
Mechi za kufuzu zitakamilika mwezi Septemba mwaka huu kabla ya droo kuandaliwa Oktoba.
Kindumbwendumbwe cha 34 cha AFCON kitaanza kutifua vumbi nchini Ivory Coast Januari 13 mwaka ujao, huku fainali yake ikisakatwa Februari 11.
Mataifa saba yametinga fainali hizo yakiwa wenyeji Ivory Coast, mabingwa watetezi Senegal, Morocco, Afrika Kusini, Algeria, Tunisia na Burkina Faso.