Katibu katika Wizara ya Fedha Dkt. Chris Kiptoo amekanusha madai kuwa Wakenya wanatozwa ushuru wa kiwango cha juu.
Wakosoaji wa serikali ya Kenya Kwanza wanataja ushuru mbalimbali ulioanzishwa na serikali hiyo tangu ilipoingia madarakani wakitoa mfano wa ada ya nyumba.
Hivi karibuni, huenda pia wakagharimika zaidi kupitia michango iliyoongezwa kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii, SHIF na Hazina ya Malipo ya Kustaafu, NSSF.
Hata hivyo, akizungumza katika mkutano wa siku tatu wa serikali ulioandaliwa mjini Naivasha kuhusu hatua za kimaendeleo za serikali, Dkt. Kiptoo alisema kuwa ni vyema nchi hii kuzalisha mapato kwa ajili ya kujitegemea kimaendeleo.
Kulingana naye, Wakenya millioni 20 wana nambari maalum ya ulipaji ushuru, lakini ni chini ya Wakenya million 8.5 wanaolipa ushuru.
Alisisitiza umuhimu wa kuuelimisha umma kuhusu masuala ya ulipaji ushuru akisema kiwango cha ushuru wanachotozwa Wakenya bado ni cha chini ikilinganishwa na mataifa mengine.
Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa kitovu cha shutuma kutoka kwa upinzani na Wakenya kwa jumla kutokana na kile wanachokisema ni kiwango cha ushuru inachowatoza tangu ichukue hatamu za uongozi.
Hata hivyo, Rais William Ruto amesisitiza umuhimu wa nchi hii kujitegemea kifedha kupitia mapato yanayokusanywa na serikali.
Ruto anasema hii ndio njia ya pekee ya kuikomboa nchi hii kutokana kwa minyororo ya madeni ambayo yameathiri kasi ya maendeleo.