Timu ya taifa ya soka ya wasichana wasiozidi umri wa miaka 17, Junior Starlets itawakaribisha wenzao wa Burundi ugani Ulinzi katika duru ya pili ya mechi ya mwisho ya kufuzu kwa dimba la dunia litakaloandaliwa katika Jamuhuri ya Dominika hapo baadaye.
Kwenye duru ya kwanza iliyochezwa nchini Uhabeshi, Kenya iliipiku Burundi magoli matatu kwa sufuri na kujawa na matumaini ya kufuzu.
Iwapo Burundi wana ndoto ya kufuzu, basi lazima washinde kwa mabao manne kwa yai, na iwapo watafunga matatu, basi wataenda kwenye muda wa ziada kisha matuta iwapo matokeo yatabaki vilevile.
Mchuano huo hautatozwa malipo huku mashabiki lukuki wakitarajiwa kuhudhuria kwa sababu ya fursa kubwa waliyonayo vipusa hao na pia kufuatia wito wa Waziri wa Michezo Ababu Namwamba wa kuwataka wajitokeze kwa wingi.
Malango ya uwanja huo yatafunguliwa saa tatu usubuhi na kufungwa punde uwanja utakapofurika.