Hatima ya PNU katika Azimio kujulikana Alhamisi

Martin Mwanje
2 Min Read

Chama cha PNU kitaamua Alhamisi wiki hii ikiwa kitasalia katika muungano wa Azimio au la. 

Ikiwa kitaupiga teke muungano huo unaoongozwa na Raila Odinga, basi kitakuwa cha pili kufikia uamuzi huo.

Chama cha Narc Kenya kinachoongozwa na Martha Karua tayari kimeanza mchakato wa kutalikiana na Azimio.

“Alhamisi ijayo, tutakuwa na kikao cha NEC (Kamati Kuu ya Kitaifa) ya chama cha PNU ambapo tutaamua msimamo wetu kama chama kuhusu uhusiano wetu na muungano wa Azimio,” amesema kiongozi wa PNU Peter Munya.

“Kwa sababu gani, kwa sababu, ile chama cha ODM ambayo ilikuwa chama kwa hii muungano wamejiunga na serikali. Na kama wamejiunga na serikali, hawawezi kuwa kwa serikali na pia wawe kwa upinzani. Kwa hivyo, kama Azimio imekuwa sehemu moja ya serikali, sisi ambao tunataka kukaa upinzani lazima tujitenge ndio tuweze kuendelea kutetea wananchi wa Kenya.”

Wanachama wa ODM walioteuliwa kuwa Mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza ni John Mbadi (Waziri wa Fedha), Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama cya Ushirika) na Hassan Joho (Waziri wa Madini).

Ni hatua ambayo imesababisha migawanyiko katika muungano wa Azimio huku vyama tanzu vikitishia kuondoka kwenye muungano huo.

Ingawa wanachama wake wameteuliwa kuwa mawaziri, kiongozi wa ODM Raila Odinga anashikilia kuwa chama hicho hakijajiunga na serikali.

TAGGED:
Share This Article