Shirika la kimataifa la Kiislamu lisilokuwa serikali limeripotiwa kulipa shilingi milioni 129 kwa lengo la kumwokoa Mkenya Stephen Munyakho almaarufu “Stevo” aliyehukumiwa kifo nchini Saudi Arabia.
Hii ni kufuatia ombi la moja kwa moja kutoka kwa Rais William Ruto.
Katibu Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar amesema Stevo anatazamiwa kurejea nyumbani baada ya fedha hizi kulipwa na shirika hilo kwa jina “The Muslim World League”.
Kulingana na Omar, ombi la kuachiliwa kwa Stevo limekubaliwa, taarifa ambayo imethibitishwa na Balozi wa Saudi Arabia nchini Kenya na Balozi wa Kenya nchini Saudi Arabia.
Katibu Mkuu huyo wa UDA aliyasema hayo jana Jumanne usiku wakati wa chakula cha jioni cha Iftar walichoandaliwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Omar ametoa wito kwa Wakenya katika mataifa ya nje kujifahamisha na sheria za mataifa hayo ili kuepuka kujipata matatani.
Stevo ni mwanawe mwanahabari mkongwe Dorothy Kweyu.
Alipatikana na hatia ya kuua bila kukusudia mwezi Oktoba mwaka 2011, hukumu ambayo ilibatilishwa baadaye na mahakama ya Kiislamu nchini Saudia.