Hassan Omar athibitishwa kuwa kaimu Katibu Mkuu wa UDA

Tom Mathinji
1 Min Read
Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha UDA Hassan Omar Hassan.

Msajili wa vyama vya kisiasa Ann Nderitu, amethibitisha rasmi uteuzi wa Hassan Omar kuwa kaimu Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), na kuchukua mahala pa Cleophas Malala aliyeshikilia wadhifa huo tangu mwezi Februari mwaka 2023.

Kupitia ujumbe kwa chama hicho, Nderitu alikubalia mabadiliko ya hivi punde katika chama hicho, huku akiagiza UDA kufanya uchaguzi katika muda wa miezi sita ijayo kuhakikisha maafisa wote wa chama hicho wanachaguliwa, ikizingatiwa kuwa maafisa wa sasa wanahudumu kwa masharti ya kukaimu.

Wakati huo huo, msajili huyo wa vyama vya kisiasa, aliagiza chama cha UDA kumtangaza katibu Mkuu huyo mpya kupitia angalau gazeti moja la hapa nchini na katika tovuti ya chama hicho, kuambatana na sehemu ya 20 ya sheria ya vyama vya kisiasa ya mwaka 2011.

Mnamo Agosti 2, 2024, Baraza Kuu la chama cha UDA, lilifutilia mbali uteuzi wa Malala kuwa katibu mkuu wa chama hicho na kumvisha jukumu hilo Hassan Omar.

Mkutano wa Baraza hilo Kuu, uliongozwa na mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Gavana wa Embu Cecily Mbarire.

Share This Article