Timu ya taifa ya Soka ya Kenya,Harambee Stars imekwea nafasi sita kwenye msimamo wa dunia wa FIFA wa mwezi Septemba uliotangazwa Alhamisi.
Kenya iliimarika baada ya kusajili ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Namibia, katika mechi ya kundi J kufuzu kwa fainai za AFCON mwaka 2025, na pia kutoka sare tasa dhidi ya Zimbabwe.
Stars imepanda kutoka nambari 108 hadi 102 katika msimamo huo mpya wa dunia.
Uganda ingali bora Afrika Mashariki katika nafasi ya 90, baada ya kuchupa kwa nafasi tano huku Tanzania ikiimarika kwa nafasi tatu hadi nambari 110.
Morocco ingali ya kwanza Afrika katika nafasi ya 14,ikifuatwa na Senegal iliyo ya 21 na Misri ikiwa ya 31, huku mabingwa wa Afrika Ivory Coast wakishikilia nambari 33, nayo Tunisia inahitimisha tano bora.
Mabingwa wa dunia Argentina,Ufaransa na mabingwa wa Ulaya Uhispania wanashikilia nafasi za 1,2 na 3 mtawalia.
Uingereza ni ya nne huku Brazil ikikamilisha nafasi tano bora ulimwenguni.