Kenya imepoteza alama mbili muhimu baada ya kukabwa koo bao 1-1 na Burundi, katika mechi ya kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia mwaka 2026, iliyochezwa Ijumaa jioni katika uwanja wa Bingu Jijini Lilongwe, Malawi.
Harambee Stars ilipata bao lake katika dakika ya 72 kupitia Duke Abuya, aliyeingia katika kipindi cha pili, kabla ya Sudi Abdallah kuisawazishia Burundi katika dakika ya 83.
Kufuatia matokeo hayo, kikosi hicho cha Engin Firat kimesalia katika nafasi ya tatu katika kundi F, ikiwa na alama 4 baada ya kucheza mechi tatu.
Harambee stars ilikuwa imeshindwa mabao 2-1 na Gabon kwenye mechi yao ya kwanza ya kundi F, kabla ya kuilemea Ushelisheli mabao 5-0 kwenye mechi ya pili ya kufuzu.
Kenya itamenyana na mabingwa wa Bara Afrika Ivory Coast Jumanne juma lijalo.