Timu ya taifa ya soka ya Kenya kwa wachezaji wanaosakata soka barani Afrika pekee imewasili jijini Kampala, Uganda mapema leo Alhamisi. Timu hiyo imewasili jijini humo kwa mechi ya marudio ya raundi ya kwanza kufuzu kwa michuano ya CHAN mwakani dhidi ya Sudan Kusini.
Mechi hiyo itapigwa kesho alasri katika uwanja wa Nelson Mandela huku Kenya inayonolewa makali na Engin Firat, ikilenga kulipiza kisasi baada ya kukomolewa mabao 2-0 na Sudan Kusini katika mkumbo wa kwanza wikendi iliyopita mjini Juba.
Licha ya Kenya kufuzu kwa fainali za CHAN mwaka ujao kama wenyeji, ni sharti washiriki mechi za kufuzu kama njia ya maandalizi.
Kenya itaandaa fainali za CHAN mapema mwaka ujao pamoja na Tanzania na Uganda kama matayarisho kwa maandalizi ya kipute cha AFCON mwaka 2027.