Harambee Stars wateleza nchini Guinea

Vijana wa Benni McCarthy sasa wataangazia mechi ya tatu ya kundi D watakapozuru Afrika Kusini tarehe 11 mwezi ujao wakishikilia nafasi ya tatu kwa alama moja pekee.

Dismas Otuke
1 Min Read

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars, ilishindwa bao moja kwa bila na wenyeji Guinea katika mchuano wa pili kundini D uliosakatwa jana Alhamisi usiku uwanjani Septemba 28 mjini Conakry.

Guinea walipata bao pekee kunako dakika ya 32 kupitia kwa mshambulizi Serhou Guirassy, anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya Borusia Dortmund nchini Ujerumani.

Wenyeji Syli Nationale walitawala kipindi cha kwanza cha mchezo na kubuni takriban nafasi tatu za kufunga mabao.

Kenya walirejea vyema kipindi cha pili kwa kuwa na asilimia kubwa ya umiliki wa mpira ingawa walikosa kumakinika katika nafasi mbili za kufunga magoli walizobuni.

Vijana wa Benni McCarthy sasa wataangazia mechi ya tatu ya kundi D watakapozuru Afrika Kusini tarehe 11 mwezi ujao wakishikilia nafasi ya tatu kwa alama moja pekee.

Harambee Stars wanatumia mechi za kufuzu kujipiga msasa kwani tayari wamejikatia tiketi kwa dimba la mwaka ujao la AFCON kama mojawapo ya waandalizi watatu pamoja na Uganda na Tanzania.

Share This Article