Hakuna afisa yeyote wa serikali wala mtumishi wa umma atakayeruhusiwa kushiriki hafla za uchangishaji fedha, almaarufu Harambee.
Marufuku hiyo inakuja wakati ambapo maafisa wa serikali hasa wabunge wametuhumiwa kwa kupora pesa za umma wanazotumia kutoa michango ya mamilioni ya pesa katika hafla mbalimbali za uchangishaji fedha/Harambee katika maeneo yao ya uwakilishi ili kupata uungwaji mkono wa wapiga kura.
“Hakuna afisa wa serikali au mtumishi wa umma atakayeshiriki hafla za umma za uchangishaji fedha/Harambee kuanzia sasa,” alitangaza Rais William Ruto wakati akilihutubia taifa leo Ijumaa.
“Mwanasheria Mkuu ameagizwa kuandaa na kuwasilisha sheria kwa misingi hii na kuandaa mkakati wa michango kutolewa kwa mpangilio na uwazi kwa madhumuni ya umma na uhisani.”
Wakenya wamewalaani vikali wabunge ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakijionyesha hadharani wakibeba mafungu makubwa ya mamilioni ya pesa za kutolewa katika hafla za michango.
Wengi wametilia shaka chanzo cha fedha hizo.