Hamtudai chochote kwa sasa, Wizara ya Fedha yawajibu Magavana

Martin Mwanje
1 Min Read
John Mbadi - Waziri wa Fedha

Serikali za kaunti zimepokea mgao wake wa fedha unaopaswa kutolewa kufikia sasa.

Akiwajibu Magavana ambao awali walitishia kusimamisha shughuli za serikali za kaunti katika kipindi cha siku 30 zijazo kutokana na ukosefu wa fedha, Waziri wa Fedha John Mbadi amesema jumla ya shilingi bilioni 158.024 zimetolewa kwa serikali za kaunti kufikia wakati huu.

Fedha hizo zinajumuisha deni la mwezi Juni pamoja na mgao wa fedha wa mwezi Julai, Agosti, Septemba na Oktoba mwaka huu.

Kulingana na Mbadi, malipo yote kwa serikali za ugatuzi yametolewa isipokuwa ya mwezi huu wa Novemba ambao bado haujakamilika.

Waziri ameyasema hayo katika taarifa saa chache baada ya Baraza la Magavana leo Jumatatu kutishia kusitisha utoaji huduma kwa  wananchi ikiwa Bunge la Taifa na lile la Seneti hayatatatua mzozo kuhusu kiasi cha fedha kinachopaswa kutolewa kwa serikali za kaunti.

Huku Seneti ikitaka kaunti kupewa mgao wa takriban shilingi bilioni 400, Bunge la Taifa linashikilia kuwa ni shilingi bilioni 380 zinazopaswa kutolewa kwa serikali za kaunti.

Hali hiyo imemfanya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kutoa wito kwa mabunge hayo mawili kusuluhisha tofauti zao na fedha kutolewa haraka iwezekanavyo kwa kaunti ili kutolemaza utoaji huduma kwa raia.

 

Share This Article