Hamisa Mobetto ampongeza mumewe kwa mkataba na Wydad

Hamisa aliambatana na mume wake Aziz Ki hadi Morocco alikotia saini mkataba na klabu ya Wydad.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji na mwanamuziki wa Tanzania Hamisa Mobetto amempongeza mume wake ambaye ni mcheza soka Aziz Ki kwa kutia saini mkataba na klabu ya Wydad Athletic ya Morocco.

Misa alichapisha picha zinazomwonyesha akiwa ameandamana na Aziz katika hafla ya kutia saini mkataba huo na kuandika, “Hongera kwa hatua hii kubwa ya kusaini mkataba wako mpya na Wydad.”

Mama huyo wa watoto wawili aliendelea kumsifia mume wake akisema kwamba huwa anaona juhudi zake, bidii yake na tamanio lake la kuwa mchezaji bora sio tu Afrika ila duniani.

“Dua na kujituma kwako ndio msingi wa mafanikio yako siku zote” Alimhimiza.

Hamisa alisema pia kwamba Aziz ni mfano wa uthubutu, uvumilivu na maono yaliyojaa matumaini kwani kila siku unapoamka huwa ana njaa ya mafanikio na hilo linampa nguvu kama mke wake.

“Kama mkeo, rafiki yako wa karibu na shabiki wako wa kwanza, dua yangu kila siku ni ufanikiwe zaidi ya ukubwa unaouota kila mara” aliendelea kusema Hamisa.

Kabla ya hapo Hamisa alikuwa amechapisha picha akiwa na watu aliowarejelea kuwa wa familia yake wanaoaminika kuwa jamaa za Aziz.

Aziz Ki amekuwa kichezea klabu ya Yanga inayoshiriki ligi kuu nchini Tanzania na sasa amehamia Wydad ya Morocco.

Website |  + posts
Share This Article