Hamas yalaumu Israel kwa makosa makubwa ya kivita

Marion Bosire
2 Min Read
Mashambulizi ya Israel dhidi ya Hamas katika eneo la Gaza.

Kundi la Hamas limelaumu Israel kwa kile linachokitaja kuwa makosa makubwa ya kivita kufuatia shambulizi la Jumamosi katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat ambapo wanajeshi wa Israel waliokoa mateka wanne.

Kulingana na hamas, shambulizi hilo lilisababisha vifo 274 na watoto wapatao 64 ni kati ya waliouawa lakini Israel imekanusha madai hayo.

Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na kundi la Hamas inasema kwamba wapalestina wengine 700 walipata majeraha kwenye shambulizi hilo la Israel.

Huku hayo yakijiri, waziri wa masuala ya kivita wa Israel Benny Gantz alitangaza kujiuzulu kwake kutoka kwa serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Akihutumbia wanahabari Jumapili Juni9, 2024, Gantz alisema kwamba Netanyahu anawazuia kuafikia ushindi kamili dhidi ya kundi la Hamas ndiposa wameamua kujiondoa kwenye serikali.

Gantz alisema kwamba amejawa na huzuni nyingi kwa hatua aliyochukua lakini anajiaminia huku akimtaka Netanyahu kuandaa uchaguzi haraka iwezekanavyo ili wananchi wa Israel wapate serikali watakayoamini.

Mwezi uliopita Gantz alitishia kujiondoa kwenye serikali ya dharura iliyobuniwa ili kuendesha vita vya Gaza iwapo Netanyahu angekosa kuwasilisha mpango wa baada ya vita wa eneo la Gaza.

Mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 37, tangu vita vilipoanza Oktoba 7, mwaka jana kama njia ya kulipiza kisasi shambulizi la Hamas ndani ya Israel.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *