Hali ya watoto njiti yamliza msanii Mrisho Mpoto

Marion Bosire
1 Min Read
Mrisho Mpoto, Msanii Tanzania

Msanii wa muziki nchini Tanzania Mrisho Mpoto ameonekana kwenye kanda ya video akilia machozi kutokana na hali ya watoto njiti hospitalini.

Mpoto aliguswa na mahitaji ya wodi ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati wa ujauzito kukamilika katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.

Anaonekana akiwa amebeba baadhi ya vitu alivyotoa mchango kwa wodi hiyo, anafuta machozi huku daktari akimpa maelezo kamili ya mahitaji.

Kama sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kusaliwa, Mpoto alizuru hospitali hiyo ambapo alitoa vitu mbali mbali vinavyohitajika kwenye wodi hiyo vya thamani ya shilingi milioni 10 za Tanzania.

Baada ya kusikia mahitaji ya watoto hao ili waweze kuishi, Mpoto aliwataka Watanzania wamuunge mkono kwani mahitaji ya watoto njiti ni makubwa sana.

Kwenye akaunti yake ya Instagram, Mpoto alichapisha picha akiwa na wahudumu wa hospitali ya Amana na kuandika, “Katika siku yangu leo ya kuzaliwa nimepata nafasi ya kutembelea Wodi ya watoto NJITI katika Hospitali ya Amana na kutoa kile nilichobarikiwa na Mungu.”

Alishukuru wote walioandamana naye kwenye ziara hiyo, walioifanikisha na wote waliomtakia heri njema maishani kwenye siku yake ya kuzaliwa.

Mpoto ametimiza umri wa miaka 46 na anafahamika sana kwa mashairi yake na kwa kutembea bila viatu.

Share This Article