Hakuna ushahidi unaothibitisha Afrika Kusini iliipatia silaha Urusi – uchunguzi

Martin Mwanje
3 Min Read
Rais Cyril Ramaphosa alisema madai hayo yameharibu sarafu ya Afrika Kusini na hadhi ya kimataifa

Uchunguzi huru haujapata ushahidi wowote kwamba Afrika Kusini ilisambaza silaha kwa Urusi, Rais Cyril Ramaphosa amesema.

Jopo hilo lilipinga madai yaliyotolewa na balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini kwamba meli ya Urusi iliwekwa risasi na silaha mjini Cape Town Desemba mwaka jana.

Madai hayo yamezua maswali juu ya madai ya kutoegemea upande wowote katika vita na Ukraine.

Bw Ramaphosa alisema kuwa imeharibu sarafu na sifa ya taifa hilo.

“Jopo liligundua kuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai kwamba meli hiyo ilisafirisha silaha kutoka Afrika Kusini kwenda Urusi,” rais alisema katika hotuba yake kwa taifa Jumapili.

“Hakuna kibali kilichotolewa cha kuuza silaha nje ya nchi na hakuna silaha zilizosafirishwa nje ya nchi.”

Uchunguzi huo badala yake ulibaini kuwa meli ya mizigo ya Urusi ilisafirisha shehena ya silaha kutoka Urusi hadi Afrika Kusini, iliyoagizwa mnamo 2018.

Madai ya Balozi Reuben Brigety yaliashiria kutia nanga kwa meli ya Lady R katika kambi ya wanamaji ya Simon’s Town kati ya tarehe 6 na 8 Desemba 2022.

Aliambia kikao cha wanahabari mjini Pretoria mwezi Mei kwamba “anaamini” silaha na risasi zilipakiwa kwenye meli hiyo “ilipokuwa ikirejea Urusi”.

Siku moja baadaye, wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini ilisema Bw Brigety “aliomba radhi” kwa kutoa madai hayo.

Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya mkutano huo, Bw Brigety alisema “anashukuru kwa fursa ya… kurekebisha maoni yoyote ya kupotosha yaliyotokana na kauli niliyotoa hadharani”.

Bw Ramaphosa aliamuru uchunguzi huru unaoongozwa na jaji kufuatia maoni ya Bw Brigety.

“Hakuna hata mtu mmoja kati ya wale waliotoa madai haya anaweza kuthibitisha madai yaliyokuwa yametolewa dhidi ya nchi yetu,” Bw Ramaphosa alisema kufuatia hitimisho la uchunguzi.

Rais atakuwa akitoa tu muhtasari mkuu wa ripoti hiyo, kwa sababu za kiusalama.

Jopo la uchunguzi huo lilitembelea kambi ya wanamaji, kuzungumza na karibu watu 50 na kukagua zaidi ya hati 100, Bw Ramaphosa aliongeza.

Afrika Kusini imejaribu kudumisha uhusiano wa kirafiki na Urusi tangu ilipovamia Ukraine Januari 2022, katika hatua ambayo imekosolewa vikali na Marekani na mataifa mengine ya Magharibi.

Ni moja kati ya mataifa machache ambayo hayakushiriki kura ya Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo huo, na kukataa kuilaani hadharani Urusi kuhusu suala hilo.

Marekani iliwahi kuhoji mazoezi ya pamoja ya jeshi la wanamaji wa Urusi na Afrika Kusini.

Share This Article