Mmoja wa viongozi wa magenge yenye nguvu zaidi nchini Haiti anasema atafikiria kuweka chini silaha ikiwa makundi yenye silaha yataruhusiwa kushiriki mazungumzo ya kuanzisha serikali mpya.
Vikundi vinavyoongozwa na Jimmy Chérizier, anayejulikana pia kama Barbecue, vinadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Port-au-Prince.
Alitabiri ghasia ambazo zimeikumba Haiti katika wiki za hivi karibuni zinaweza kuongezeka katika siku zijazo.
Hata hivyo, aliiambia Sky News: “Tuko tayari kwa suluhu.”
Haiti, taifa maskini la Karibea lenye watu zaidi ya milioni 11, imekuwa bila Waziri Mkuu tangu Machi 12.
Ariel Henry alijiuzulu baada ya kuzuiwa na magenge yenye silaha kurejea kutoka Kenya, ambako alikuwa ametia saini mkataba wa kuagiza kikosi cha kulinda amani cha kijeshi kutoka nje ya nchi kwa nia ya kurejesha utulivu.
Baraza la Mpito la Rais limeanzishwa ili kuandaa mpango wa kurudisha Haiti kwenye utawala wa kidemokrasia, ukiungwa mkono na mataifa mengine ya Karibea na Marekani.
Chérizier, mtu mashuhuri zaidi katika muungano wa magenge unaojulikana kama Viv Ansanm, ambao unadhibiti karibu asilimia 80 ya mji wa Port-au-Prince, anaamini kundi lake linafaa kuwa na kiti katika meza ya mazungumzo siku zijazo.
Aliiambia Sky News: “Ikiwa jumuiya ya kimataifa itakuja na mpango wa kina ambapo tunaweza kuketi pamoja na kuzungumza, lakini hawalazimishi kile tunachopaswa kuamua, nadhani kwamba silaha zinaweza kupunguzwa.”
Alisema “hajisikii fahari” ya ghasia zinazoendelea nchini Haiti, na akaonya kwamba mgogoro unaweza kuendelea ikiwa makundi kama yake, ambayo yanapinga “wanasiasa wafisadi”, hayatakuwa sehemu ya serikali ya baadaye.
Pia alisema vikosi vyovyote vya Kenya vilivyoandaliwa nchini humo ili kuimarisha usalama vitachukuliwa kuwa “wavamizi”.