Hafla za Hollywood zaahirishwa huku makazi ya watu maarufu yakiharibiwa na moto

Hatua hii inafuatia mkasa wa moto ambao umechoma makazi mengi ya watu maarufu ambao ni wahusika wakuu wa hafla hizo.

Marion Bosire
1 Min Read

Mkasa wa moto unaokumba sehemu kadhaa za Los Angeles nchini Marekani umesababisha kuahirishwa kwa hafla kadhaa za Hollywood wakati huu wa tuzo mbali mbali za kila mwaka.

Hafla ya kutoa tuzo za wakosoaji almaarufu Critics Choice Awards iliyokuwa imepangiwa kuandaliwa mwishoni mwa juma hili imeahirishwa kwa wiki mbili.

Matangazo ya walioteuliwa kuwania tuzo za hadhi ya juu za Oscar pia yameahirishwa kwa muda wa siku mbili kulingana na waandalizi.

Matayarisho ya vipindi mbali mbali vya runinga yalisimamishwa kikiwemo kipindi cha Jimmy Kimmel Live na Grey’s Anatomy huku uzinduzi wa filamu nyingi tu ukisimamishwa.

Mamlaka ya jiji pia imezuia watu wasifike karibu na eneo maarufu la jina la Hollywood katika vilima vilivyo juu ya Los Angeles.

Watu kadhaa maarufu wametangaza kuharibiwa kwa makazi yao na moto huo ulioanzia kwenye msitu na kuenea hadi kwa makazi ya kifahari.

Walioathirika ni pamoja na mwigizaji Adam Brody na mkewe Leighton Meester ambaye pia ni mwigizaji, Billy Crystal, Paris Hilton na Ashton Kutcher.

Wengine ni Ricki Lake, Eugene Levy, Manduy Moore na James woods.

Mchekeshaji Gina Yashere pia aliathirika lakini anasema kwamba ana bahati kwani ana eneo mbadala la kuishi huko Costa Rica.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *