Hafla ya kumkumbuka Mzee Jaramogi Oginga Odinga yatangazwa

Marion Bosire
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kisumu Profesa Peter Anyang Nyong’o ametangaza kwamba kutakuwa na hafla ya kumkumbuka mzee Jaramogi Oginga Odinga.

Kupitia ukurasa wake uliothibitishwa wa Facebook, Gavana Nyong’o ameelezea kwamba hafla hiyo itaandaliwa Jumamosi Januari 20, 2024, katika kanisa la Mtakatifu Stephen ACK eneo la Milimani.

Ibada hiyo ya ukumbusho ya miaka 30 tangu kifo cha mzee huyo imepangiwa kuanza saa nne asubuhi na baadaye mchana kutakuwa na kikao cha hotuba katika ukumbi wa Ofafa jijini Kisumu.

Gavana Nyong’o amealika wote ambao wanaweza kufika siku hiyo kujiunga na familia katika kutoa shukrani na kumkumbuka mpendwa wao.

Kulingana na Nyong’o, Mzee Jaramogi Oginga Odinga ni mmoja wa viongozi wa kitaifa nchini ambao walibuni mwelekeo wa taifa hili.

Aliyekuwa mhadhiri wa somo la historia katika chuo kikuu cha West Virginia nchini Marekani Robert Maxon ni mmoja wa watakaohutubu siku hiyo.

Maxon kwa upande wake amesema anatizamia kuzungumza kwenye hafla hiyo akisema kusema ukweli ni sehemu ya urithi wa Mzee Jaramogi Oginga Odinga.

Jaramogi Oginga Odinga ambaye ni babake kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliaga dunia Januari 20, 1996 akiwa na umri wa miaka 82.

Aliwahi kuhudumu kama makamu wa Rais kati ya mwaka 1964 na mwaka 1966.

Share This Article