Hafla ya kuaga waliofia kwenye maporomoko ya jumba Tanzania kuandaliwa leo

Marion Bosire
1 Min Read

Hafla ya kuaga watu 13 waliofariki katika ajali ya kuporomoka kwa jengo moja katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam itaandaliwa leo Novemba 18, 2024.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alitangaza hayo na kuongeza kwamba shughuli hiyo itaandaliwa katiwa uwanja wa Mnazimmoja jijini Dar es Salaam na itaanza saa saba mchana hadi saa kumi jioni.

Akizungumza usiku wa kuamkia leo, Chalamila alisema shughuli ya kuaga miili hiyo itaongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku Ndugu wa waathiriwa wakitakiwa kukutana katika Hospitali ya Amana saa mbili asubuhi kwa ajili ya taratibu mbalimbali.

Chalamila alifafanua pia kwamba zoezi la uokoaji litaendelea na kwamba wameamua kuaga miili hiyo kutokana na ushauri wa madaktari.

Ajali hiyo ilitokea Jumamosi Novemba 16, 2024 na kufikia sasa wapo ambao wameokolewa kutoka kwenye vifusi huku jumla ya miili 13 ikiondolewa katika eneo la tukio.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alitoa taarifa jana kutoka Brazil ambapo anaendeleza ziara rasmi, na alibainisha kwamba waliookolewa ni watu 84, kufikia jana saa nne asubuhi.

Wote waliookolewa walifikishwa hospitali kwa matibabu wengi wakaruhusiwa kwenda nyumbani huku 26 wakilazwa kwa matibabu zaidi.

Rais Samia alisema serikali itagharamia matibabu pamoja na mazishi ya waliofariki.

Share This Article