Mabingwa wa ligi kuu nchini Gor Mahia wametangaza kupiga marufuku usajili wachezaji wa kigeni, baada ya kufungiwa nje ya kipute cha ligi ya mabingwa Afrika msimu ujao.
Mwenyekiti wa Gor Ambrose Rachier amesema madhara yaliyoletwa na wachezaji hao ni mengi na watakuwa wakisajili wachezaji wa humu nchini pekee.
Timu hiyo imekuwa ikiwasajili wachezaji wa kigeni kila msimu kama njia ya kuwa na kikosi thabiti.
Wachezaji watatu wa kigeni akiwemo kipa wa Mali Adama Keita, mshambulizi wa Burundi Jules Ulimwengu na mshambulizi wa Congo Sando Yangayaw, waliishtaki Gor kwa FIFA baada ya kukosa kulipwa malimbikizi ya mishahara yao kulingana na mkataba na kusababisha Gor kupigwa marufuku kushiriki mashindano ya Afrika.
Rachier amesema uamuzi huo umeafikiwa kwa pamoja na usimamizi wa klabu kama tahadhari.