Gor Mahia na Police FC kazi ipo dhidi Mafarao wikendi hii

Dismas Otuke
2 Min Read

Gor Mahia  na Police FC zote za humu nchini zitakabiliwa na kibarua kigumu katika  mkumbo wa kwanza mchujo wa pili, kuwania kombe la Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho mwishoni mwa juma hili dhidi ya wapinzani wa Misri katika uga wa taifa wa Nyayo.

Limbukeni Police FC watakuwa na mlima wa kukwea watakapokabiliana na mabingwa watetezi Zamalek ya Misri Jumamosi kuanzia saa tisa alasiri kiwarani Nyayo, katika kombe la Shirikisho ikiwa mechi ya kwanza baina ya timu hizo mbili.

Zamalek SC

Police  wanaonolewa na kocha Anthony Kimani walifuzu kwa mchujo wa pili, baada ya kuwabwaga Ethiopia Coffe bao moja kwa nunge.

Upande wao Zamalek waliotwaa kombe hilo msimu jana kwa kuishinda RS  Berkane ya Morocco, katika fainali watakuwa wakishiriki kwa mara ya kwanza msimu huu, baada ya kupeushwa awamu ya mchujo.

Upande wao Gor  Mahia watashuka Nyayo Stadium Jumapili kuanzia saa tisa juu ya alama, kushikana mashati na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika,Al Ahly ya Misri katika duru ya kwanza ya mchujo wa pili.

Mabingwa wa Kenya mara 21, Gor walifuzu kwa raundi hii baada ya kuwasasambua El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini, jumla ya magoli 5-2 kwenye mchujo wa kwanza.

Al Ahly SC

Ahly maarufu kama Red Devils wamenyakua mataji 12 ya Ligi ya Mabingwa na kombe moja la shirikisho.

Mechi za marudio zitaandaliwa wiki ijayo nchini Misri huku washindi wa jumla wakifuzu kwa hatua ya makundi.

Share This Article