Gianluigi Buffon aamua kutundika daluga

Francis Ngala
2 Min Read

Golikipa mashuhuri raia wa Italia Gianluigi Buffon ametangaza kustaafu soka na kutia kikomo taaluma hiyo miaka 28 baadaye.

Buffon mwenye umri wa miaka 45 alichezea klabu ya Parma msimu uliopita na anachukua uamuzi huo kutokana na majeraha ambayo yamekuwa tatizo katika kuendeleza taaluma yake ya soka.

Akiwa na Parma msimu uliokamilika, Gianluigi Buffon alikaa nje kwa miezi mitatu kutokana na majeraha ya misuli, huku klabu yake ikishindwa kupanda daraja hadi Serie A, sababu kuu inayotajwa kuwa huenda ikawa chanzo cha kustaafu kwake.

Buffon alijiunga na Parma kwa mara ya pili msimu wa mwaka 2021 akiwa na matumaini ya kuirejesha katika daraja la Serie A lakini hilo halikutimia katika misimu miwili ambayo ameitumikia klabu hiyo inayoshiriki ligi ya Serie B nchini Italia.

Buffon anastaafu akiwa na umri wa miaka 45. Photo/Footballtalk

 

Alishiriki mechi 45 katika mara ya pili klabuni hapo lakini akakumbwa na majeraha msimu uliopita. Msimu uliopita wa mwaka 2022/23, alicheza mara 19 pekee.

Katika kipindi cha maisha yake ya soka, Buffon ameshinda mataji 10 ya Serie A, sita ya Supercoppa Italiana, sita ya Coppa Italia na Kombe la Dunia mwaka 2006 akiwa na Italia.

Vile Vile Gianluigi Buffon anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi zaidi katika ligi ya Serie A, ambapo ameshiriki michezo  657.

 

Website |  + posts

I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.

Share This Article