Prof. Naana Jane Opoku-Agyemang ndiye Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke nchini Ghana kufuatia uchaguzi ulioandaliwa wiki jana.
Prof. Opoku alikuwa mwaniaji mwenza wa Rais mteule John Dramani Mahama, aliyeibuka mshindi kwa tiketi ya chama cha National Democratic Congress (NDC) .
Ushindi huo ni hatua kubwa na pia ushindi mkubwa kwa wanawake nchini Ghana.
Awali, Prof. Opoku aliandikisha historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Cape Coast mwaka 2008.
Baadaye mwaka 2013, aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu katika serikali ya Rais Mahama, kabla ya kuteuliwa mwaniaji mwenza wa Mahama katika chama cha NDC mwaka 2020.
Mahama anarejea tena katika Ikulu kuiongoza Ghana kwa muhula wa pili, baada ya kuwa usukani kati ya Julai mwaka 2012 na Januari mwaka 2017.