Gereza la Kisii kuhamishiwa kwingine

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki amesema kwamba serikali kuu itahamisha gereza la Kisii kutoka katikati ya mji hadi sehemu iliyo nje ya mji huo.

Akizungumza alipozuru gereza hilo leo asubuhi, Kindiki alisema hatua hiyo inalenga kurahisisha mipangilio ya mji huo mkuu wa kaunti ya Kisii na kutoa nafasi kwa miradi mbalimbali ya serikali kuu na serikali ya kaunti.

Kindiki alikuwa ameandamana na wakuu wa masuala ya usalama katika kaunti ya Kisii alipozuru jela hiyo kujifahamisha kuhusu ilipofikia mipango ya uhamisho.

Rais William Ruto alifichua mipango ya kuhamisha jela hiyo mwaka jana wakati wa sherehe ya kukaribishwa nyumbani kwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Alisema lengo lake ni kupata eneo la kupanua mji wa Kisii ambao kulingana naye umesongamana sana na akasema kwamba upanuzi huo ulitegemea juhudi za viongozi wa kaunti za kutafuta eneo mbadala la kuweka gereza.

Akiwa katika gereza la Kisii, Waziri Kindiki alizungumzia visa vya vurugu ambavyo vimeshuhudiwa awali katika kaunti ya Kisii hasa kwenye mikutano ya kisiasa.

Amesema serikali itachukua hatua kali dhidi ya vijana ambao wanatumiwa na wanasiasa kuzua vurugu na wanasiasa ambao watapatikana na hatia ya kufadhili vijana kama hao pia wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Share This Article