Mwanamuziki wa Uganda Gen Mega Dee anayeishi Marekani ametangaza kwamba amehitimu kama daktari.
Dee alihamia Marekani mwaka 2017 akiwa na ari ya kusomea kozi ya udaktari ambapo alitia bidii na kumaliza masomo ya shahada ya usimamizi na uongozi katika masuala ya afya mwaka 2021.
Hakuachia hapo bali aliendelea na kozi ya kumfuzisha kabisa kuhudumu kama daktari nchini Marekani safari ambayo sasa imekamilika.
Alitangaza habari hizo njema kupitia akaunti yake ya Facebook ambapo aliandika, “Leo Oktoba 30, 2024, nimekuwa Daktari KIGENYI AMOS baada ya kukamilisha mahitaji yote ya kimasomo.”
Mwanamuziki huyo aliendelea kusema kwamba amewezeshwa kuafikia hayo na Mungu, familia, nidhamu na bidii.
Mega Dee alikuwa anamiliki kampuni ya muziki kwa jina Afande Records UG na anafahamika kwa wimbo “Obudde” na “Woman Of My Life”.
Anaripotiwa kumiliki kliniki iitwayo Kind Love Healthcare Agency nchini Marekani.