Gavana Waiguru alalamikia mauaji ya wanawake nchini

Martin Mwanje
1 Min Read

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru amelalalamikia idadi inayoongezeka ya mauaji ya wanawake nchini na kutoa wito kwa polisi kusitisha mauaji hayo mara moja.

Waiguru hasa ametoa wito kwa taasisi za upelelezi kuharakisha uchunguzi juu ya kiini cha mauaji hayo na kuwawajibisha wahusika.

Kulingana na mwenyekiti huyo wa zamani wa Baraza la Magavana, hatua hiyo itasaidia kukomesha kutokea kwa mauaji hayo nchini.

Anasema taifa hili limepigwa na butwaa kutokana na ripoti za mara kwa mara za mauaji ya kutatanisha ya yanayotokea yamkini kila siku kote nchini.

Gavana huyo aliyasema hayo wakati wa hafla ya mazishi ya Seth Nyakio Njeri ambaye ni bintiye Mwakilishi Wadi mteule wa Bunge la Kirinyaga Lucy Njeri.

Njeri alipatikana akiwa ameuawa katika mtaa wa Biafra mjini Thika Oktoba 14 mwaka huu.

Maoni yake yanakuja wakati ambapo Chama cha Mawakili Wanawake, FIDA kimelalamikia vikali mauaji yanayoongezeka ya wanawake nchini yanayoshuhudiwa kwa sasa.

Chama hicho kimetoa wito kwa Rais William Ruto kutangaza mauaji hayo kuwa janga la kitaifa na kuchukua hatua mara moja kuyakomesha kabla mambo hayajakwenda mrama.

Share This Article