Gavana wa zamani Sospeter Ojaamong ateuliwa mwenyekiti wa NEPAD

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amemteua aliyekuwa gavana wa kaunti ya Busia Sospeter Ojaamong kuwa mwenyekiti wa bodi simamizi ya shirika la ushirikiano mpya wa maendeleo barani Afrika NEPAD na tawi la Kenya la shirika la umoja wa Afrika kuhusu tathmini ya utaratibu wa maendeleo – African Peer Review Mechanism (APRM).

Kulingana na tangazo katika gazeti rasmi la serikali, uteuzi wa Ojaamong ni kuanzia Ijumaa Juni14, 2024 na atahudumu kwa muhula wa miaka mitatu.

Katika wadhifa huo, Ojaamong atakuwa na jukumu la kuratibu miradi yote ya NEPAD katika wizara mbali mbali, kaunti, idara, mashirika, washirika wa kimaendeleo na wadau wengine.

Lengo kuu la NEPAD ni kuliweka bara Afrika katika njia ya maendeleo endelevu na kutafuta kukomesha kutengwa kwa maeneo fulani barani humu.

Teuzi zingine zilizofanywa na Rais Ruto ni pamoja na uteuzi wa Albert Chege kama mwenyekiti wa baraza la taasisi ya michezo ya Kenya, uteuzi wa Patricia Ithau kama mwenyekiti wa hazina ya maendeleo ya milenia ya Kenya na Bernadette Nganga kama mwenyekiti wa bodi ya wahariri wa kitabu cha mwaka cha Kenya.

Profesa Ratemo Waya Michieka pia ameteuliwa kuwa chansela wa chuo kikuu cha Tharaka na wote hao watahudumu katika nyadhifa zao kwa muda wa miaka mitatu.

Website |  + posts
Share This Article