Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati ndiye Naibu Mwenyekiti mpya wa Kitaifa wa chama cha ODM.
Arati anajaza pengo lililoachwa na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Kisii Janet Ong’era aliyejiuzulu wadhifa huo.
Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Busia Catherine Omanyo ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa ODM.
Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Busia Florence Mutua ambaye pia alijiuzulu wadhifa huo.
Mbunge wa Mlima Saboti Caleb Amisi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mratibu wa chama kurithi nafasi ya aliyekuwa Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kwale Zulekha Hassan.
Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Kakamega Elsie Muhanda ameteuliwa kuwa Katibu wa Usalama wa chama kuchukua nafasi ambayo awali ilishikiliwa na mbunge wa zamani wa Shinyalu Justus Kizito.
Seneta wa kaunti ya Migori Eddie Oketch ameteuliwa kuwa Katibu wa Masuala ya Binadamu na Usimamizi wa Masuala ya Majanga.
Mabadiliko hayo yanafuatia mkutano wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama cha ODM uliofanyika juzi Jumatano.
Wakati wa mkutano huo, wabunge watano waasi na wawakilishi wadi wanne katika kaunti ya Kisumu walifurushwa kwa utovu wa nidhamu na kukiuka itikadi za chama.