Gavana Sakaja atoa hatimiliki 912 kwa wakazi wa Nairobi

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana Sakaja atoa hatimiliki kwa wakazi wa Nairobi.

Ni afueni kwa wakazi wa kaunti ya Nairobi, baada ya Gavana Johnson Sakaja kutoa hatimiliki 912 za kumiliki ardhi.

Hatimiliki hizo zilitolewa kwa wakazi wa mitaa 14 wa kaunti hiyo, ambao kulingana na Sakaja, haiwapi tu fursa ya kumiliki ardhi  lakini pia wanalindwa dhidi ya wanyakuzi wa ardhi.

Mitaa hiyo ni pamoja na  Kayole, Soweto,  Dandora, Matopeni Spring Valley, Patanisho, Pumwani na Mathare North.

Mitaa mingine ni Pumwani,  Komarock, Jua Kali Sector B iliyoko  Kariobangi South, KCC  iliyoko Mowlem, Umoja One na Umoja Innercore.

Wakati wa hafla hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Charter Hall Jijini Nairobi, Sakaja alikariri kujitolea kwa utawala wake katika kutimiza ahadi yake ya kuangazia suala la utoaji hati miliki.

Alisema katika kipindi Cha miaka miwili iliyopita, serikali ya kaunti ya Nairobi ilitoa hati miliki 7,000 kwa wakazi na taasisi zilizoko kwenye kaunti hiyo.

“Ni jukumu letu kama serikali kuwahudumia. Hadi sasa tumetoa hatimiliki 7,000 katika muda wa miaka miwili. Leo tumetoa hatimiliki 912 kwa wakazi wa Nairobi,” alisema Gavana Sakaja.

Sakaja alisistiza kuwa mpango huu ni moja ya mikakati iliyowekwa ili kuboresha utoaji huduma.

Wakati huo huo, Gavana Sakaja alielezea wasiwasi kuhusu unyakuzi wa ardhi iliyotengewa watoto kucheza, akitoa hakikisho kuwa itawaliwa na serikali yake.

“Ukosefu wa hatimiliki huwaweka wamiliki halisi wa ardhi katika hatari ya kuhadaiwa na wanyakuzi na wastawishaji wa kibinafsi,” alidokeza Gavana Sakaja.

Website |  + posts
Share This Article