Gavana Sakaja atetea mpango wa lishe shuleni

Marion Bosire
1 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja

Gavana wa jimbo la nairobi Johnson Sakaja ametetea mpango wa lishe shuleni katika kaunti yake akisema katika shule ambazo zilikuwa zimesajiliwa kwenye mpango huo katika awamu ya kwanza, wanafunzi wamekuwa wakipokea chakula moto na kwa wakati.

Haya yanajiri baada ya mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kukosoa uendeshaji na usimamizi wa mpango huo. Kulingana naye, chakula hakijakuwa kikifikia walengwa kwa wakati suala ambalo linavuruga ratiba ya masomo.

Sakaja sasa anasema kwamba ni wanasiasa wanaojitakia makuu katika kaunti ya Nairobi ndio wanatia doa mpango wake wa lishe shuleni.

Anasema lengo lao ni kujipigia debe kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ambao alisema bado uko mbali sana.

Kulingana naye, mpango huo wa “Dishi na County” ni lazima ufanikiwe na ni lazima watoto wa Nairobi wakule, washibe, wanone na wasome.

Serikali ya kaunti ya Nairobi ilijenga majiko ya kisasa katika shule 10 za sehemu mbali mbali za kaunti ya Nairobi ambapo chakula hutayarishwa kufaidi watoto wa shule hizo huku chakula kingine kikisafirishwa hadi shule ambazo zimeorodheshwa.

Kila mwanafunzi huhitajika kulipa shilingi tano kila siku ili kupata chakula hicho.

Kumekuwa na malalamishi katika mitandao ya kijamii kwamba wanafunzi hawajakuwa wakipata chakula hicho hata baada ya kulipia huku wengine wakichelewa kukipokea.

Share This Article