Gavana wa kaunti ya Narok Patrick Ole Ntutu ametetea hatua ya serikali ya kaunti ya kuongeza ada ya kuingia katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara akisema lengo ni kuboresha huduma humo.
Ntutu alisema kuongezwa kwa ada hiyo kutoka shilingi 9, 205 hadi 26,300 kwa kila mtu msimu wa watalii wengi ni hatua ya kimakusudi inayolenga kuwezesha utawala wake kumudu usimamizi wa mbuga hiyo.
Aliongeza kwamba watalii hulipa dola 1000 hadi 2000 kulala usiku mmoja katika hoteli zilizoko Maasai Mara, dola 500 kubebwa na puto la moto na dola 200 kwa siku kujionea wanyamapori na hivyo ada iliyoongezwa haifai kuwa tatizo.
Kiongozi huyo wa kaunti ya Narok alisema watalii wanaozuru mbuga hiyo hawaendi pale kulala bali kujionea wanyamapori na hakuna vile kulala kunaweza kuwa ghali kuliko kujionea wanyama.
Alilaumu waendesha biashara huko Mara na wanablogu kwa kueneza habari za uongo kwamba watalii waliokuwa wakilenga Maasai Mara wamebadili na kuelekea mbuga ya Serengeti nchini Tanzania.
Gavana alisema habari hizo ni za kupotosha kwani hata hoteli za mbuga ya Maasai Mara zimejaa kabisa kwa muda wa miezi miwili ijayo.
Ole Ntutu alisema alihusisha wadau wote kabla ya kutangaza nyongeza ya ada ya kiingilio ya Maasai Mara na alipata uungwaji mkono hasa kutoka kwa madereva na waongoza ziara.