Gavana wa kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti ametoa wito kwa kiongozi wa nchi Rais William Ruto kutafakari vilivyo kabla ya kuteua mawaziri.
Akizungumza jana Jumapili katika kanisa la katoliki la Mtakatifu Jude huko Athi River, kaunti ya Machakos, Wavinya alisema wakenya wanamtizamia Rais kuteua watu wenye uadilifu kama mawaziri.
Ndeti alitambua kwamba hakuna binadamu mkamilifu lakini sasa Rais ana muda mwafaka wa kutambua na kuteua watu walio na ujuzi unaohitajika kwa nyadhifa za mawaziri.
Rais William Ruto alivunja baraza la mawaziri hivi maajuzi na kurasimisha kupitia arifa ya gazeti rasmi la serikali kuondolewa kwa mawaziri 21 afisini.
Ijumaa alitangaza watu 11 ambao amewateua kama mawaziri na kuahidi kukamilisha uteuzi kwa wakati.
Wakati huo huo, askofu wa dayosisi ya Nakuru ya kanisa katoliki Cleophas Oseso ametupilia mbali mabadiliko ambayo Rais Ruto amefanyia baraza la mawaziri akiyataja kuwa bandia.
Akizungumza na wanahabari jana, Askofu Oseso alisema kwamba uteuzi aliofanya Rais wa mawaziri 11 haukuridhisha wengi huku akimlaumu kwa kurejesha waliokuwa kwenye baraza la awali la mawaziri.
Oseso anahisi kwamba Rais angeteua watu tofauti kabisa wenye ujuzi ambao wangemsaidia kubadilisha uchumi wa nchi hii na kurejesha imani ya wakenya katika utawala wake.
Askofu Oseso sasa anawarai wabunge kukatalia mbali wasiostahiki nyadhifa za mawaziri wakati watakuwa wanawasaili bungeni.
Kiongozi huyo wa dini ameonyesha kutoridhishwa kwake pia na pendekezo la kubuni serikali ya umoja wa kitaifa akisema hatua hiyo itaathiri demokrasia.