Gavana wa kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya ameelezea hatua alizochukua tangu alipoingia madarakani ili kuleta mabadiliko makubwa katika kaunti hiyo kwa manufaa ya raia.
Amesema miezi 18 iliyopita, alishika hatamu za uongozi wakati wakazi walikuwa wamepoteza matumaini katika uwezo wa serikali ya kaunti hiyo kuwatumikia kama taasisi ya kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Mifumo yetu ya afya ilikuwa kitovu cha ufisadi, mapato yaliyokusanywa yalikuwa ya kiwango cha chini na yaliwafaidi watu wachache mabwanyenye na upatikanaji wa huduma kama vile maji safi, barabara, mwanga, na masoko kwa ajili ya mazao yetu ulionekana kama upendeleo na mifumo ya serikali ilikuwa hafifu kiasi kwamba ufikiaji wa malengo ya ugatuzi ilikuwa ndoto tu,” alisema Gavana Natembeya katika hotuba yake kwa bunge la kaunti hiyo.
Kulingana naye, sasa mambo yamebadilika kutokana na ahadi yake aliyoitoa Agosti 25, 2022 kwa wakazi kuwa angebadilisha mambo kwa manufaa yao.
Gavana Natembeya anasema utawala wake umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wakulima ambao ni asilimia 60 ya wakazi wa kaunti hiyo wananufaika na kilimo chao.
Ili kuhakikisha hilo, alisema serikali yake ilianzisha mpango wa utoaji mbegu za ubora wa hali ya juu na mbolea bila malipo kwa wakulima ili kuhakikisha kaunti hiyo inajitosheleza kwa chakula.
Mpango huo, kulingana naye, pia umesaidia kuwakinga wakulima dhidi ya pembejeo za bei ghali.
“Tunawapongeza wawakilishi wadi ambao wameunga mkono mpango huu na wamehakikisha watu wao wamepata bidhaa hizi,” alisema Gavana Natembeya akitoa mfano wa wadi za Nabiswa, Chepchoina na Kwanza.
Aliongeza kuwa chini ya mpango huo, wakulima wadogo zaidi ya 900,000 wamenufaika katika awamu ya kwanza na hatua hiyo kusababisha ongezeko la mahindi yaliyovunwa kwa magunia 300,000 katika msimu uliopita wa upanzi.
Huku akielezea kuwa kumekuwa na ongezeko la vyama vya akiba na mikopo almaarufu SACCOs katika kaunti hiyo hususan mjini Kitale, Gavana Natembeya pia alisisitiza umuhimu wa vyama hivyo katika kuchochea maendeleo.
“Katika kutambua vyama hivyo na mahitaji yanayoongezeka ya mikopo ya gharama nafuu inayotolewa kwa watu, serikali yangu imeanzisha usajili wa vyama vya ushirika na mikopo katika wadi zetu zote 25,” aliongeza Natembeya.
Wala hakukomea hapo. Aliangazia pia sekta ya elimu akitoa mfano wa maendeleo yaliyopatikana katika kuhakikisha ufanisi wa shule za chekechea.
Kwa mujibu wa Gavana huyo, shule 437 za chekechea zmeanzishwa zikiwa na wanafunzi 37,745 na walimu 791 kufikia mwezi Novemba mwaka jana. Kati ya walimu hao, alisema 738 wameajiriwa kwa masharti ya kudumu na kwamba mchakato wa kuwaajiri walimu waliosalia kwa masharti yayo hayo unaendelea.
Nyanja zingine ambazo Gavana Natembeya aligusia katika hotuba yake yenye kurasa 40 ni afya, maji, tabia nchi na kadhalika.