Hazina ya Nawiri inayokusudia kuhakikisha vijana, wanawake, watu wanaoishi na ulemavu na wengineo wanaepukana na vikwazo vya kiuchumi vinavyowazuia kufikia ndoto zao maishani imezinduliwa katika kaunti ya Trans Nzoia.
Hazina hiyo yenye kima cha shilingi milioni 80 ilizinduliwa na Gavana George Natembeya wakati wa hafla iliyoandaliwa katika uwanja wa maonyesho ya kilimo mjini Kitale leo Ijumaa.
“Ni muhimu kutambua kuwa, tangu uhuru, ukuaji wa biashara katika kaunti yetu umezuiwa na vikwazo vilivyopo sasa kama vile; ukosefu wa kuunga mkono miundombinu ya kijamii, kifedha na miundombinu kama vile barabara,” alisema Gavana Natembeya.
“Biashara katika kaunti yetu imekumbana na changamoto kama vile utamaduni hasi wa ujasiriamali, na kuwa kizuizi cha kuanzisha biashara.”
Gavana Natembeya alitaja ukosefu wa ujuzi stahiki, ukosefu wa masoko ya kutosha na nafasi za kufanya biashara kuwa baadhi ya changamoto ambazo lazima zipigwe teke ili kaunti hiyo iweze kunawiri kibiashara.
Chagamoto anazosema serikali yake tayari imezishughulikia ipasavyo tangu iliposhika hatamu za uongozi.
Alitoa mfano wa kukamilishwa kwa ujenzi wa masoko ya mazao yanayotolewa shambani katika maeneo ya Kapkarwa, Weonia, Mitume, Kapkoi na Kachibora.
“Hii yote inakusudia kumpatia mama mboga wetu na wafanyabiashara wengine wadogo nafasi ya kufanya biashara kwa heshima na kujivunia,” aliongeza Gavana Natembeya.
Isitoshe, alisema ujenzi wa soko la Masinde Muliro utakamilika na kuzinduliwa katika kipindi mwaka mmoja ujao.
Hazina ya Nawiri
Wakazi wengi wa kaunti ya Trans Nzoia kwa muda mrefu wamekumbana na tatizo la kupata mikopo ya gharama nafuu, hali ambayo imekuwa pigo kwa ukuaji wa biashara katika kaunti hiyo.
Ni tatizo hili ambalo lilikuwa chanzo cha Hazina ya Nawiri.
Hazina hiyo itatoa mikopo kwa watu watakaonufaika kwa wastani wa shilingi 200,000 kwa kila ombi litakalokubaliwa.
Mikopo hiyo itatozwa riba ya asilimia 3 na inapaswa kulipwa katika kipindi cha mwaka mmoja.
Na ili kuboresha usimamizi wa hazina hiyo, Bodi ya Hazina ya Nawiri imeanzishwa kwa mujibu wa sheria ya hazina hiyo.
“Tuna imani kwamba timu hii ina ujuzi unaohitajika kuwakilisha ipasavyo na kuwahudumia vijana, wanawake, mashirika ya biashara, vyama vya akiba na mikopo na makundi mengine,” Gavana Natembeya alibubujikwa na matumaini.