Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza amewasili katika majengo ya bunge tayari kwa kikao chha kusikiliza mashtaka ya kutimuliwa kwake.
Anakabiliwa na mashtaka 7 waliotumia Wawakilishi Wadi kumtimua mamlakani.
Mashtaka hayo ni pamoja na ubadhirifu wa rasilimali za kaunti, ukabila na mienendo inayokiuka maadili, unyanyasaji na kuwadunisha viongozi wengine, uteuzi unaokiuka sheria, kudharau mahakama na kulidharau bunge la kaunti ya Meru.
Kikao cha kusikiliza mashtaka dhidi ya Gavana Mwangaza kitaandaliwa na bunge la Seneti leo Jumanne na kesho Jumatano.
Hii ni mara ya pili kwa bunge la Seneti kuamua hatima ya Gavana Mwangaza baada ya bunge hilo kumnusuru awali.
Gavana Mwangaza amekuwa akikwaruzana na Wawakilishi Wadi wa kaunti ya Meru mara kwa mara, na juhudi za kuwapatanisha hazijazaa matunda.