Gavana wa kaunti ya Bungoma Kenneth Lusaka amehakikishia Seneti kwamba akaunti zote 352 za benki za serikali ya kaunti hiyo ni halali.
Lusaka alifika mbele ya kamati ya Seneti kuhusu ugatuzi na mahusiano ya serikali mbali mbali jana baada ya msimamizi wa bajeti kutaja Bungoma kuwa moja ya kaunti ambazo zina akaunti nyingi za benki.
Spika huyo wa zamani wa Seneti alielezea kamati hiyo kwamba akaunti zote hizo zilifunguliwa kwa kibali kutoka kwa msimamizi wa bajeti na benki kuu ya Kenya.
“Nyingi ya akaunti hizi ni za taasisi za mafunzo ya kiufundi na vituo vya afya vya serikali.” alielezea Lusaka mbele ya kamati hiyo ambayo iko chini ya uenyekiti wa Seneta wa Wajir Abass Mohamed.
Alisema kati ya akaunti hizo 152 ni za taasisi za mafunzo ya kiufundi huku 146 zikiwa za vituo vya afya.
Akaunti nyingine kulingana na Lusaka ni za mapato mbali mbali ya serikali ya kaunti ya Bungoma kama vile ushuru inaokusanya.
Gavana Lusaka alisema hospitali za kaunti hiyo ya Bungoma hipokea ufadhili moja kwa moja kutoka kwa wafadhili na hivyo ni muhimu ziwe na akaunti za benki.
Abass aliomba ripoti kamili ya majina ya wanaosimamia akaunti hizo zote za benki ili kamati ipate ufahamu zaidi.