Gavana wa kaunti ya West Pokot Simon Kachapin amelinyoshea Bunge la Seneti kidole cha lawama kutokana na kile ambacho amekitaja kuwa kushindwa kuhakikisha kaunti zinapokea mgao wake wa fedha.
Amesema hatua hiyo imekuwa chanzo cha mateso ya kaunti ambazo hazina fedha za kuendesha shughuli zake.
Gavana Kachapin hususan amewashutumu Maseneta Samson Cherargei wa Nandi na Julius Murgor wa West Pokot kwa kukosoa utendakazi wa serikali za kaunti kila mara.
Alimshutumu Cherargei kwa kuzielezea kaunti kama mfumo uliovunjika akilalama kuwa si vyema kwa Maseneta kuwataka Magavana kufika mbele yao kujibu maswali mara kwa mara.
Kulingana naye, ni wajibu wa mabunge ya kaunti kuangazia utendakazi wa serikali za kaunti.
Kadhalika, Gavana Kachapin amepuuzilia mbali ripoti ya Mdhibiti wa Bajeti iliyoitaja kaunti ya West Pokot kuwa miongoni mwa kaunti 10 ambazo hazijatumia fedha zozote kutekeleza miradi ya maendeleo katika robo mwaka ya kwanza ya kati ya mwezi Julai na Septemba.
Anasema hakujakuwa na maendeleo yoyote katika kaunti tangu mwezi Julai kwa sababu kaunti hazikupatiwa fedha.